13 Januari 2024 - 12:49
Medvedev: Kupeleka Uingereza askari wake Ukraine kutamaanisha kutangaza vita dhidi ya Russia

Dmitry Medvedev, Naibu Mkuu wa Baraza la Usalama la Russia amesema, kupelekwa askari wa jeshi la Uingereza nchini Ukraine kutakuwa sawa na kutangaza vita dhidi ya Russia.

Akizungumzia ziara ya Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak nchini Ukraine, rais huyo wa zamani wa Russia amekumbusha kwamba kiongozi huyo mkuu wa Uingereza amekuja kuonyesha uungaji mkono kwa Ukraine, siku chache baada ya Kyiv kuushambulia kwa makombora mji wa Belgorod wa Russia kwa mabomu ya vishada. "Umma wa Magharibi ungesema nini kama ujumbe wa Uingereza ungeshambuliwa kwa mabomu ya vishada katikati mwa Kyiv kama ilivyotokea kwa raia wa Belgorod yetu?" amehoji Medvedev. Medvedev, ambaye aliwahi kuwa rais wa Russia kati ya mwaka 2008 hadi 2012, ameiita Uingereza "fidhuli na "adui wa milele" wa Russia.Naibu Mkuu wa Baraza la Usalama la Russia amefafanua kwa kusema: "natumai adui wetu wa milele, Uingereza jeuri, inaelewa kuwa kupeleka kikosi chao rasmi cha kijeshi nchini Ukraine kutamaanisha kutangaza vita dhidi ya nchi yetu".

 Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak jana Ijumaa alitembelea Kyiv na kutangaza msaada wa kijeshi wa pauni bilioni 2.5 (karibu dola bilioni 3.1) kwa Ukraine katika mwaka ujao wa fedha, lengo likiwa ni kuimarisha uwezo wa ulinzi wa nchi hiyo kupitia teknolojia ya kisasa. Sambamba na ziara hiyo ya Sunak mjini Kiev, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ametangaza kuwa nchi yake na Uingereza zimesaini makubaliano ya ushirikiano wa kiusalama wa miaka 10  wa kiwango "kisio na kifani".../

342/